Thursday, January 18, 2018

VIGOGO WIZARA MALIASILI, UTALII KORTINI KWA TUHUMA ZA KUSABABISHA HASARA DOLA 32,599

Na Karama Kenyunko, Glogu ya jamii

WAFANYAKAZI watatu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka sita likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya dola 32,599.

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(Takukuru) Leonard Swai, amewataja washtakiwa hao ni, Ofisa Muhifadhi anayehusika na uwindaji wa matumizi endelevu ya wanyamapori Rajabu Hochi, Ofisa wa Muhifadhi mwenye wajibu wa kukusanya wa mapato ya uwindaji , Mohamed Madehele na Isaac Maji.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri imedaiwa kuwa, washtakiwa wakiwa watumishi kitengo cha Wanyamapori, walitenda makosa hayo katika makao makuu ya wizara hiyo.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali Pendo Temu amedai,kati ya Januari 12 na Desemba 31, mwaka 2008, makao makuu ya wizara hiyo, Hochi na Madehele wakiwa watumishi wa wizara hiyo, wakiwa na wajibu wa kukusanya mapato yanayotokana na uwindaji walitumia madaraka yao vibaya kwa kuzidisha wanyama pori kwa Kampuni ya Uwindaji ya Northern Hunting Enterprises (Tanzania) kinyume cha sheria na hivyo kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida ya USD 250 isivyo halali.

Pia Hochi na Madehele, wanadaiwa kati ya Agosti 11 na Desemba 31, mwaka 2011, makao makuu ya wizara hiyo,waliiwezesha kampuni hiyo kujipatia dola za Marekani 250 isivyo halali.Aidha, Hochi na Madehele, wanadaiwa, kati ya Septemba 5 na Desemba 31,mwaka 2010, walishindwa kukusanya faini ya dola za Marekani 15,630 kutoka katika kampuni hiyo.

Pia washtakiwa Hochi na Madehele,wanadaiwa kushindwa kukusanya faini ya dola za Marekani 250 kutoka kampuni ya uwindaji ya Hunting Enterprises (Tanzania), kinyume cha sheria.

Pia kati ya Oktoba 12, 2008 na Desemba 31,mwaka 2011, Hochi na Madehele walishindwa kukusanya mapato yatokanayo na uwindaji dola za Marekani 16,219 kutoka kampuni ya uwindaji ya Hunting Enterprises (Tanzania) na hivyo kuiwezesha kampuni hiyo kupata mapato hayo isivyo halali.

Katika shtaka la sita, washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 12, 2008 na Desemba 31,mwaka 2011, katika makao makuu ya wizara hiyo, wakiwa na wajibu wa kukusanya mapato yatokanayo na uwindaji, waliisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 32,599.

Hata hivyo, washtakiwa wote wamekana mashtaka na wamesomewa masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili watakao saini bondi ya Sh.milioni 50 na mmoja kati ya wadhamini anatakiwa kuweka hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh.milioni 50.


Pia washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na imeahirishwa hadi Januari 31, mwaka huu itakapotajwa tena.

No comments: