Monday, November 20, 2017

BENKI YA KILIMO YATEMBELEA MIRADI YA JKT KITEULE CHA BULAMBA, BUNDA

Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetembelea mradi wa ufugaji wa vifaranga vya samaki unaotekelezwa na kikosi cha 822 Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Rwamkoma wilaya ya Butiama kupitia Kiteule chake cha Bulamba, wilayani Bunda.

Akizungumza lengo la ziara hiyo, mkuu wa msafara huo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila amesema lengo kubwa la kutembelea Mradi huo ni kujionea juhudi za serikali za kuchagiza mapinduzi ya kilimo hasa katika tasnia ya ufugaji na uvuvi wa samaki nchini.

Bibi Kurwijila aliongeza kuwa tasnia ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa ufugaji wa samaki nchini.

Aliongeza kuwa Benki ya Kilimo imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa Ufugaji wa Samaki na uvuvi nchini ili ziweze kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.

Mradi huo wa ufugaji wa samaki unaotekelezwa na JKT Wilaya ya Bunda, Kiteule cha Bulamba ulizinduliwa rasmi mwezi Novembea, 2014 kwa kupandikiza vifaranga vya samaki katika vizimba ndani ya Ziwa Victoria.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo Economic Social Research Foundation (ESRF) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Ufugaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria, umekuwa maarufu zaidi katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Uganda na Kenya ambapo umepunguza kwa kiasi kikubwa uvuvi haramu katika fukwe za ziwa hilo.
 Afisa Kilimo na Ufugaji wa kikosi cha 822 Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Rwamkoma, Kapteni M. Kinana (kulia) akiongea na Ujumbe kutoka Benki ya Kilimo (hawapo pichani) walipotembelea mradi huo uliopo wilayani Bunda. Kushoto ni Msimamizi wa Mradi wa Ufugaji wa Samaki wa JKT Kiteule cha Bulamba, Luteni Kelvin Gondo.
 Maafisa wa Jeshi la Kujenga Taifa wanaotekeleza Mradi wa Ufugaji wa Samaki kwa Vizimba Kiteule cha Bulamba wakifuatilia mkutano wa pamoja kati ya JKT na Ujumbe kutoka Benki ya Kilimo.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bibi Rosebud Kurwijila (kulia) akizungumza wakati walipotembelea Mradi wa Ufugaji wa Samaki kwa Vizimba Kiteule cha Bulamba uliopo wilaya ya Bunda, Mkoani Mara. Kushoto ni Afisa Uvuvi wa wilaya ya Bunda, Bw. Steven Ochieng’.
 Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TADB, Bw. Dome Malosha (kulia) akizungumza wakati walipotembelea Mradi wa Ufugaji wa Samaki kwa Vizimba Kiteule cha Bulamba uliopo wilaya ya Bunda, Mkoani Mara. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila (kushoto) na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Bw. Joseph Mutashubilwa (katikati).
 Afisa Uvuvi wa wilaya ya Bunda, Bw. Steven Ochieng’ (kushoto) akichangia wakati wa mazungumzo hayo. Anayemsikiliza ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila (kulia).
Msimamizi wa Mradi wa Ufugaji wa Samaki wa JKT Kiteule cha Bulamba, Luteni Kelvin Gondo akitoa maelezo juu ya maendeleo ya ufugaji wa samaki katika hatua mbalimbali.

No comments: