Saturday, July 22, 2017

BALOZI WA ISRAEL NCHINI MHE. YAHEL VILAN AWAAGA WAFANYAKAZI WA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) BAADA YA KUMALIZA MUDA WAKE WA KUFANYA KAZI HAPA NCHINI


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimshukuru Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Yahel Vilan (kulia) kutokana na nchi yake kuisaidia Taasisi hiyo kuwapatia mafunzo madaktari, wauguzi na kutoa matibabu kwa watoto. Katikati ni Daktari Bingwa wa Moyo kwa watoto na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo Sulende Kubhoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Yahel Vilan wakati alipotembelea Taasisi hiyo leo kuwaaga wafanyakazi baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi hapa nchini. Israel imekuwa ikiisadia JKCI kwa kutoa mafunzo kwa madaktari, wauguzi na matibabu kwa watoto.
Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Yahel Vilan akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati alipotembelea Taasisi hiyo leo kuwaaga wafanyakazi baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi hapa nchini. Israel imekuwa ikiisadia JKCI kwa kutoa mafunzo kwa madaktari, wauguzi na matibabu kwa watoto.
Mwanamuziki kutoka nchini Israel Maestro Nir Brand akiwaimbia wimbo watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati balozi wa nchi hiyo Mhe. Yahel Vilan alipotembelea Taasisi hiyo kuwaaga wafanyakazi baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi hapa nchini.
Balozi wa Israel nchini ambaye makazi yake yapo Nairobi nchini Kenya Mhe. Yahel Vilan (watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi pamoja wa wafanyakazi wa Taasisi hiyo na wageni kutoka nchini Israel.
Daktari Bingwa wa Moyo kwa watoto na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo Sulende Kubhoja wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) akizungumza na Daktari Bingwa wa mfumo wa chakula kwa watoto Cohen Shlomi kutoka nchini Israel wakati wa ziara ya balozi wa nchi hiyo alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuwaaga wafanyakazi.
Baadhi ya watoto wanaotiba katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Balozi wa Israel nchini ambaye makazi yake yapo Nairobi nchini Kenya Mhe. Yahel Vilan alipokuwa akiwaaga wakati wa ziara yake aliyoifanya leo katika Taasisi hiyo. Serikali ya Israel kupitia Taasisi ya Save Child Heart (SACH) imegharamia matibabu ya watoto 40 tangu Novemba 2015 hadi sasa ambao walitibiwa nchini humo.
Balozi wa Israel nchini ambaye makazi yake yapo Nairobi nchini Kenya Mhe. Yahel Vilan akizungumza na wafanyakazi pamoja na watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakati wa ziara yake ya kuwaaga aliyoifanya leo baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi hapa nchini. Israel imekuwa ikiisadia Taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa madaktari, wauguzi na matibabu kwa watoto.

Picha na JKCI

WAZIRI LUKUVI AONYA MAAFISA ARDHI WASIO WAADILIFU


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwaonya maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusababisha kero za migogoro ya ardhi nchini wakati wa uzinduzi Master Plan ya mji wa Iringa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimkabidhi kitabu cha Master Plan ya mji wa Iringa Meya wa Halmashauri ya Iringa Alex Kimbe.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiteta jambo na Meya wa Halmashauri ya Iringa Alex Kimbe na Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akipongezwa na Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa mara baada ya Uzinduzi wa Master Plan ya mji wa Iringa.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Iringa waliofika kushuhudia Uzinduzi huo.

……………………………………………………………………………………….

Na Hassan Mabuye Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ardhi


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amewaonya maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusababisha kero za migogoro ya ardhi nchini.

Waziri Lukuvi aliyasema hayo leo katika ukumbi wa shule ya sekondari Lugalo mjini Iringa wakati wa Uzinduzi wa Master Plan ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Amesema mchezo huo wa ufisadi ambao umekuwa ukitumiwa miaka yote na maofisa ardhi nchini ameubaini na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutokubaliana na ramani za maeneo mapya zinazoletwa na wataalam hao bila ya wao kufika maeneo husika na kuoneshwa maeneo hayo ili kujiridhisha.

Waziri Lukuvi amefichua kuwa ufisadi unaofanywa na maafisa ardhi nchini kwa kupima viwanja hewa kwa ajili ya maslahi yao na kusema kuwa mbinu ambayo wamekuwa wakiitumia kuiibia serikali amekwisha ibaini na hata kubali kuona mbinu hiyo inapewa nafasi katika serikali hii ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli .

Maafisa ardhi wakishirikiana na maafisa mipango miji pamoja na wapima wamekuwa wakitajirika sana kwenye idara zao na wanatakata kwa ujanjaujanja na ufisadi wanaoufanya kwa kutengeneza ramani zinazoonesha maeneo mazuri na muhimu katika miji kwamba hayafai kutumika, kumbe wameyauza maeneo hayo kwa mlango wa nyuma na kwa bei za juu.

Unakuta kwenye ramani inayonyesha kuna bonde kubwa lisilofaa kujengwa kumbe ukifuatilia eneo hilo ni zuri kuliko yote na hapo wametenga viwanja vya kuuza. Unakuta ukipima kuna viwanja vingi na vizuri ambavyo ni vyao wao wanachofanya baada ya kuuza viwanja halali za Halmashauri hurudi kupima maeneo hayo walioonyesha ni mabonde na kugawana wao kwa ajili ya kuuza kwa faida yao.Lukuvi amesema kuwa wathamini nao pi wamekuwa wakiwapunja wananchi wasio elewa kwa kuwafanyia tathimini kubwa zaidi ya uhalisia wake na pindi pesa inapotoka utakuta nyumba inathamani ya milioni 7 wakati wao wanasema inathamani ya milioni 20 ili cha juu wapate wao.

“wakati nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam niliweza kubaini ujanja wa wathamini baada ya eneo ambalo nyumba zake zina thamani kati ya milioni 20 hadi 50 kwa maana nyumba hizo ni za udongo ila maofisa hao walimtafuta mtu na kutafuta nyumba nzuri zaidi na kumshikisha kibao kisha kumpiga picha na kuandika kuwa nyumba hiyo inathamani ya zaidi ya milioni 200.

Niliamua kufanya uchunguzi wangu na kumtafuta mtu aliyekwenye picha na kumbana ndipo aliniambia ukweli kuwa mthamini huyo ni ndugu yake hivyo walikubaliana pesa ikitoka atalipwa milioni 70 na milioni 130 ni za afisa huyo”

Hata hivyo alisema kuwa ujenzi holela katika miji na halmashauri imesababishwa na ukilitimba wa utoaji wa vibali kwa wakati na ndio sababu ya wananchi kuvamia maeneo yasiyo pimwa japo kuanzia sasa wote waliopo katika maeneo yasiyo pimwa watapewa leseni ya makazi ya miaka mitano na watalipa kodi ya ardhi na baada ya miaka mitano wahakikishe wamepimiwa ili kupewa hati.

Hivyo Lukuvi aliwataka maafisa ardhi na wathamini wa ardhi manispaa ya Iringa kutofanya kama maeneo mengine kwa kufuata mpango maeneo yote ambayo yameelekezwa kwenye Masta Plan hiyo na kwenda kutenda haki.

Katika hatua nyingine waziri Lukuvi alitoa agizo kwa wale wote waliopewa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na viwanda na wale waliouziwa viwanda vya serikali, hotel na mashamba ya serikali kuviendeleza haraka kabla ya ardhi hiyo haijapokonywa .

Nae Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bibi Amina Masenza akimkaribisha waziri Lukuvi amesema kuwa mkoa wa Iringa umeendelea kuhamasisha wananchi kuzingatia sheria na taratibu za ujenzi na kuachana na ujenzi holela na ndio sababu ya kuja na Masta Plan hiyo ambayo imeanzishwa na aliyekuwa mstahiki meya wa halmashauri hiyo Amani Mwamwindi.

Akitoa taarifa ya uandaaji wa Masta Plan hiyo kwa ajili ya mwaka 2015-2035 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Dkt William Mafwere, alisema kuwa dhumuni la mpango huo ni kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili Manispaa na kuwa dhana kuu ya mpango huo ni dhana unganishi ikijumuisha dhana nyingine.

Alisema jumla ya miradi 31 itatekelezwa katika awamu ya kwanza 2015-2020 kuwa baadhi ya miradi hiyo ni kituo cha mabasi Igumbilo, kituo hicho kimeanza ujenzi na hatua ya utekelezaji imefikia asilimia 30.

Nae Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa alisema kuwa kazi inayofanywa na Waziri Lukuvi ni tofauti na mawaziri wengine kwani amekuwa ni waziri wa mfano katika kuchapa kazi.

“Kwa mnaonifahamu vizuri mimi sio mbunge wa kusifia sifia ni mbunge mwenye msimamo ila nampongeza sana Waziri Lukuvi ni waziri mchapakazi na kazi zake zinaonekana na ndio maana hata bungeni ni waziri pekee ambaye bajeti yake ilipitishwa kwa kishindo hata na sisi wabunge wa kambi ya upinzani”

Mpango Kabambe ni chombo cha kuchochea utumiaji wa fursa zilizopo katika mji, kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kupunguza na kumaliza migogoro ya ardhi. kudhibiti ujenzi holela mijini na hutumika pia kuongoza, kusimamia na kudhibiti ukuaji na uendelezaji wa mji na kutoa uhakika kwa wawekezaji katika Halmashauri za Manispaa ya husika.

KWA SIMU TOKA LONDON- Mitaani na muziki wa Kizungu

IJUE PIANO – NA MANUFAA YAKE
Na Freddy Macha 
Piano (au kinanda)  ni chombo mahsusi cha  Wazungu. Kitaaluma muziki maana yake ni vitu vitatu : melodi (unayoisikia bila hata kujua maneno na kuipigia uluzi), ridhimu (mapigo), na mpangilio wa sauti (“harmony”). Kipengele cha tatu ndiyo kigumu zaidi....
Kati ya vyombo muhimu  vya kitengo cha utunzi na upangaji (“harmony”) wa muziki ni Piano na Gitaa.
Ila Piano inaongoza Uzunguni.
 Ndiyo maana kila utakapokwenda,  makanisani, mabaa, mashuleni, majumbani na hata vituo vya usafiri hukosi Piano. Kihistoria, watunzi mashuhuri wa muziki ulimwenguni wametumia Piano kupanga vibao vyao vilivyofahamika na kupendwa miaka mingi  zaidi.
 Mifano michache  ni George Gershwin (“Summertime”- 1934),  Stevie Wonder (“Superstition”, 1973 ), Billy Joel  (“I love You Just the Way You are”- 1977) , Herbie Hancock (“Watermelon Man”, 1962), Paul McCartney ( “Nyimbo za Beatles,  “Let it Be”, “Long Winding Road”, “Yesterday”, nk), Prince (”When Doves Cry”, 1984), Gill Scott Heron (Mtunzi mashuhuri wa Mashairi aliyefariki 2011),  na  Alicia Keys , binti , kijana anayewika sasa.
Hata wanamuziki waimbaji walipiga piano, ingawa si sana hadharani. Prince, Michael Jackson, James Brown, nk.
Afrika yetu tunao marehem Fela Kuti na Abdullah Ibrahim (Afrika Kusini) anayeheshimika kama mmoja wa wapiga piano wakubwa duniani wa Jazz. Watanzania marehemu Patrick Balisidja  na Kassim Magati (Sunburst) vile vile. Miaka yake ya mwisho marehem Balisidja alipiga Piano akiwa na King Kiki.
 Kimuziki Piano ni kama kamusi. Ni muhimu kuijua kuelewa nini kinatendeka katika moyo, ngozi na mifupa  ya muziki. Kiafya upigaji Piano huoanisha pande mbili za Ubongo na kuzuia kuchakaa kwake.  Hivyo kwa Wazee na watu wa makamo ni kinga maradhi ya kusinyaa na kulemaa Ubongo mathalan “Dementia” na “Alzheimer”...
Hii ni sababu mkono  mmoja hufanya tendo tofauti na mwingine, unapotwanga Piano.
Kufuatana na maelezo ya mwanasayansi wa Kimarekani,  Roger Sperry (aliyeshinda tuzo la Nobel 1981) upande wa  kushoto wa Ubongo hufikiri,  na kulia  mambo ya hisia na utunzi. Bw Sperry alifikia ugunduzi huo akifanya utafiti wa kiini cha Kifafa.
 Ni vizuri pia kwa watoto wadogo na huwasaidia kufanya vyema katika masomo yote. Ndiyo maana muziki na Sanaa (kijumla) huzingatiwa sana mashuleni Uzunguni. 
Mwafrika jifunze Piano hata kama unaanza kuzeeka, itakufaa.  Na wasisitize wanao kufanya muziki na sanaa, utawajenga kiakili katika hesabu na sayansi pia.

 Rick Schmull akionesha vitu, mitaani London

Mdau nikionja embe. 

Mpiga piano, Billy Joel akiimba wimbo wake maarufu wa mapenzi duniani, kimaudhui na kimuziki.

Wimbo huo ulifanywa maarufu zaidi na marehemu Barry White. Ulidunda sana madisko na redio za  Afrika Mashariki enzi zake 


Mpiga Piano maarufu wa Afrika Kusini, Abdullah Ibrahim. Gwiji wa Jazz

MAGAZETI YA JUMAMOSI LEO JULAI 22,2017

Friday, July 21, 2017

DKT. MPANGO ATANGAZA MAPATO KODI YA MAJENGO SHILINGI BILIONI 32.5.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akivipongeza Vituo vya Mafuta vya Puma na Total kwa kuonesha mfano wa kufunga mashine za EFDs katika Pampu zote za mafuta kwenye vituo vyao, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.(Picha: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwaomba wananchi kulipa kodi ya Majengo mapema kwa mwaka wa Fedha 2017/18 ili kuepuka usumbufu wa msongamano, alipofanya Mkutano na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akitoa agizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha kuwa mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFDs) zinatumika ipasavyo na kutengenezwa mara moja zinapoharibika na kwamba zisipotengenezwa ndani ya saa 48 zifungwe na wamiliki wake watozwe faini, alipozungumza na wanahabari, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam wakiwa katika Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) ambapo Waziri huyo aliwashukuru wananchi kwa kulipa kodi ya Majengo kiasi cha Sh. Bilioni 32.5 kufikia Julai 15, 2017, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam.

………………………………………………………………..

Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 32.5 ya kodi ya majengo, kwa mwaka wa fedha 2016/17 kutoka katika Majiji, Miji na Manispaa 30 nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) amewaambia waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwamba makusanyo hayo ni sawa na asilimia 56 ya lengo lililowekwa Mwaka wa Fedha uliopita la kukusanya shilingi bilioni 58.

Alisema kuwa hatua niyo ni mafanikio makubwa tangu TRA ipewe jukumu la kukusanya kodi hiyo ambapo mwaka wa fedha 2015/2016 katika maeneo hayo, Halmashauri zilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.3 wakati TRA imekusanya kiasi hicho cha shilingi bilioni 32.5 tangu ianze kukusanya kodi hiyo mwezi Oktoba mwaka wa fedha 2016/2017.

“Mpaka kufikia tarehe 15 Julai mwaka huu TRA imekusanya sh. bil 32.5 kipindi ambacho ni kifupi, na kwamba mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka kutokana na mwitio mkubwa wa wananchi kulipa kodi ya majengo”Alisema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango aliwapongeza wananchi kwa mwitio wao mkubwa wa kulipa kodi ya majengo na kwamba wameonesha uzalendo wa kweli na ndio maana Serikali imeamua kuongeza muda wa kulipa kodi hiyo bila adhabu hadi Julai 30 mwaka huu, hali anayoamini itapandisha zaidi mapato hayo.

Katika hatua nyingine Dkt, Philip Mpango aliwapongeza wamiliki wa vituo vya mafuta waliotii maagizo ya Serikali, kwa kufunga mashine stahiki za EFDs, akitolea mfano vituo vya PUMA na TOTAL ambavyo vimefunga mashine hizo kwenye pampu zao zote.

Aliwaonya wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao hawatafunga mashine hizo za EFDs ndani ya siku 14 kama agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli linavyoelekeza na kwamba yeye kama Waziri mwenye dhamana atahakikisha analisimamia kikamilifu na kwamba baada ya muda huo mtu asijekuilaumu Serikali baada ya kuanza kuchukua hatua kali za kisheria.

Aliwataka wamiliki wa vituo hivyo kupitia chama chao cha wamiliki wa vituo vya mafuta TAPSOA kuheshimu maelekezo ya Serikali na kuacha majibizano yasiyo na tija kuhusu amri hiyo ya Rais kwenye vyombo vya habari kwa kuwa huo ni utovu wa nidhamu.

Aliwageukia wenye maduka ya vifaa vya ujenzi, vileo na maduka makubwa ‘supermarket’ nao watumie mashine hizo za kukusanyia mapato ya Serikali (EFDs) kikamilifu na kutoa risiti kwa wateja wao huku akiwaasa wateja nao kudai risiti wanapofanya manunuzi kulingana na kiwango halisi cha bidhaa wanazonunua.

Alipiga marufuku wafanyabiashara wanaosingizia mashine za EFDs kuwa mbovu na kuwaonesha wateja wao makaratasi waliyotoa taarifa TRA kwamba mashine zao zilikuwa mbovu kwa kipindi kifrefu na kuaigiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kusimamia jambo hilo ili kuhakikisha kuwa linakoma kabisa.

“TRA mtimize majukumu yenu mliyodhaminiwa na Serikali na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara ambao mashine zitakuwa hazitumiki ndani ya saa 48 kwa kisingizio cha kuharibika zifungiwe na wamiliki watozwe faini na kulipa kodi ya Serikali ipasavyo” aliagiza Dkt. Mpango.

“Serikali ya Awamu ya Tano haijaribiwi, tumeazimia tutafanya kazi kwa niaba ya wanyonge ili nchi yetu iende mbele na kwa hili watusamehe.” Alisisitiza Dkt. Mpango

Dkt Mpango alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kujitoa kwake kuwatumikia wananchi na kuongoza mapambano ya uchumi yatakayo ifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ambao hata watu wa kawaida watajisikia kuwa unakua kwa kutatua changamoto zao za maisha.

Alisitiza watanzania wafanye kazi kwa bidii kujenge nchi ili kila Mtanzania apate huduma bora, barabara bora, tiba nzuri, maji, yote haya hayawezi kufanyika bila mapato yakutosha na kwamba Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe.