Thursday, January 18, 2018

DK. MAHIGA AHIMIZA MAZINGIRA MAZURI KUVUTIA WAWEKEZAJI

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk.Augustine Mahiga amesema kuwa ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kutengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwamo za sheria, kodi, ajira,vvivutio vya uwekezaji na kilimo.

Dk.Mahiga, ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kuzindua kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Ubalozi wa India nchini Tanzania kwa kushirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Lengo la kongamano hilo pamoja na mambo mengine washiriki wamezungumzia namna ya ushiriki wa sasa na siku zijazo unavyoweza kuleta amani katika nchi wanachama wa jumuiya hizo.Kauli mbiu ya kongamano katika kongamano hilo inasema "Amani, utulivu na maendeleo".

Dk. Mahiga amefafanua jambo hilo si jipya kuzungumzwa isipokuwa bado halijaeleweka na hivyo linatakiwa kuzunguzwa Tanzania pamoja EAC.

“Tunamkakati madhubuti wa kujenga viwanda katika EAC na SADC. Sasa kusema nataka viwanda ni kingine, kuvuta viwanda ni kingine, kufanya viwanda vizalishe na vistawi ni jambo lingine.

"Na ukisema unataka viwanda mazingira yapo?  unataka kufanikisha viwanda je  utaalam upo? hapo sasa kupitia mambo hayo matatu unaweza kuendesha viwanda,” amesema Dk.Mahiga.

Ameongeza katika kongamano hilo watazungumzia kinadharia kuhusu amani na jumuiaya hizo zinavyochagia kuleta amani katika nchi na namna mchanganyiko wa amani unavyoweza kuleta maendeleo katika mataifa hayo yanayoshirikiana.

Amewakumbusha washiriki wa kongamano hilo kuwa "Hapa tumekumbuka mchango wa mwanaharakati mkubwa Mahatma Ghandhi aliyeliyesisimua dunia kutokana na mapambano yake na Waingereza ili kuleta uhuru wa wa India na viongozi wengi wa Afrika waliiga mfano huo na hata Hayati Mwalimu Jualias Nyerere aliwahi kusema kuwa alijifunza kutoka kwake.

Pia Dk. Mahiga amesema nchi ya India ni kubwa na ina watu zaidi ya Sh.bilioni 1.2 na wana amani na wamekuwa wakifanya uchaguzi kwa demokrasia na kubwa zaidi wamejiimarisha kiuchumi na kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake upo imara na kueleza ipo haja kwa nchi nyingine kuiga kutoka Taifa hilo.

"Amani inaweza kutazamiwa ndani ya nchi kama unatengeneza taasisi za  ushirikishi na uwajibikaji na si tu kudumisha amani bali kuleta utulivu wa kisiasa,"amesema Dk.Mahiga.

Naye aliyewahi kuwa Balozi wa Kwanza nchini India mwaka 1994 na Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, amesifu uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na India na hayo ni matunda ya Hayati Mwalimu Nyerere na Waziri Mkuu wa kwanza wa India  Jawaharial Nehru.

Kwa upande wa Balozi wa India nchini, Sandeep Arya, amesema pamoja na kujadili masuala ya ushirikiano Serikali ya India itatumia fursa ya kongamano hilo kukusanya maoni, mapendekezo na taarifa ambayo yatatolewa na washiriki waliopo na pamoja na wadau hasa wamasuala ya ulinzi, amani na maendeleo ili kila Taifa lifikie malengo ya kitaifa na kuboresha maisha ya wananchi wake.

Ameelezea namna ambavyo India imekuwa ikishirikiana na nchi zilizopo Bara la Afrika ikiwamo Tanzania katika kufanikisha upatikanaji wa maendeleo kwenye nyanja mbalimbali.
 Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwenye Kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Ubalozi wa India nchini Tanzania kwa kushirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk.Augustine Mahiga akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi Kongamano la siku mbili ambalo limeandaliwa na Ubalozi wa India nchini Tanzania.Kauli mbiu ya kongamano hilo ni Amani, Utulivu na Maendeleo.

Profesa Mbarawa awataka TPA kukamilisha na kuhamia jengo jipya

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Eng. Deusdedit Kakoko (kulia)akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Mbarawa (kushoto) alipokagua jengo jipya 'One Stop Centre' la TPA leo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo  kwa Naibu Mkurugenzi wa TPA (Miundombinu), Eng. Karim Mattaka (kushoto) alipotembelea na kukagua jengo jipya 'One Stop Centre' la TPA leo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akitoa maelekezo katika ziara ya kukagua ujenzi wa jengo jipya 'One Stop Centre' la Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) lililopo bandarini leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Eng. Deusdedit Kakoko na Naibu Mkurugenzi wa TPA (Miundombinu), Eng. Karim Mattaka wakimsikiliza.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akimsikiliza kwa makini mmoja wa abiria wa Kivuko cha Magogoni alipofanya ukaguzi wa kivuko hicho leo jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akiwasikiliza baadhi ya abiria wa Kivuko cha Magogoni alipofanya ukaguzi wa kivuko hicho leo jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akiwa na baadhi ya abiria wa Kivuko cha Magogoni mara baada ya ukaguzi wa kivuko hicho leo jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto) akisalimiana na Naibu Mkurugenzi wa TPA (Miundombinu), Eng. Karim Mattaka (kulia) mara baada ya kuwasili kukagua ujenzi wa jengo jipya 'One Stop Centre' la Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Kakoko.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo katika ziara ya kukagua ujenzi wa jengo jipya 'One Stop Centre' la Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) lililopo bandarini leo jijini Dar es Salaam. 

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kuhakikisha kazi ya kukamilisha ujenzi wa jengo jipya 'One Stop Centre' inakamilika haraka na kuanza kutoa huduma kwa mamlaka hiyo na wadau wake wote.

Akizungumza mara baada ya kukagua jengo hilo leo jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa  amesema ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam utafikiwa pale wadau wote wa bandari hiyo watakapofanya kazi saa 24 na katika eneo moja ili kumrahisishia mteja kupata huduma kwa haraka na katika kiwango kinachokubalika kimataifa.


"Natoa miezi sita kuanzia leo kwa TPA msimamieni mkandarasi  kikamilifu ili ikifika Juni muwe mmehamia ninyi na wadau wenu wote katika jengo hili," alisititiza Prof. Mbarawa katika ziara hiyo.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Deusdedit Kakoko amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati tayari yeye amehamia kwenye jengo hilo, ili kuongeza hamasa kwa mkandarasi kukamilisha ujenzi wake.


"Tumejipanga ifikapo mwezi wa nne ofisi zote zitakazotumiwa na wadau wa bandari ziwe zimekamilika ili kuruhusu baadhi ya ofisi kuanza kuhamia katika jengo hili," amesema Eng. Kakoko.


Jengo hilo la kisasa lenye ghorofa 36 ambalo litawaweka wadau wote wa bandari mahali pamoja ili kurahisisha huduma kwa wateja litagharimu takribani shilingi bilioni 143 litakapokamilika mwezi Juni mwaka huu na kutoa fursa kubwa ya uwekezaji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.


Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua huduma za Kivuko cha Magogoni na kuwataka wasimamizi wa kivuko hicho kuondoa wafanyabiashara na ombaomba ndani ya eneo la kivuko ili kuboresha usalama na kupunguza kero kwa abiria na madereva, na kuwataka abiria kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira waingiapo na watokapo katika eneo la kivuko.


Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

WATOTO WENYE SHIDA WAFAIDIKA NA BIMA YA AFYA

 Wageni wa Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini wakiangalia moja ya mradi wa ufugaji unaofadhiliwa na na Mfuko wa Abbot Tanzania katika Makao ya Taifa Dar es Salaam  aliye katikati ni Makamu wa Rais wa Mfuko wa Abbot  Bi. Jenna Daugherty.
 Baadhi ya watoto wa Makao ya Taifa ya Watoto wakiimba mbele ya wageni kutoka wafadhili wa Makao yao Abbot Tanzania pamoja na uongozi wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto jijini Dar es Salaam.
 Baaadhi ya Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  pamoja na Wafanyakazi wa Makao ya Watoto  wakifuatilia kwa makini maigizo ya Watoto wanalelewa kituoni hapo pichani ni Bi. Ferediana Kiromo kushoto na kulia kwake ni Beatrice Mwatujobe wote kutoka Wazira ya Afya.
Mlezi wa Makao ya Taifa ya Watoto Bi. Beatrice Mugubilo akiongoza wageni wa Makao yake kuangalia maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Abbot Tanzania.
Na Anthony Ishengoma.

Watoto wanaoishi katika Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini wamefaidika na huduma ya Bima ya Afya kwa ajili ya matibabu yao baada ya shirika la Abbot Tanzania kuwezesha ufadhili wa huduma hiyo muhimu pamoja kuwafungulia akaunti za benki ili waweze kumudu kulipia upya wakati bima zao zinapofikia mwisho wa muda wake.

Shirika hili limekuwa mfadhili mkuu wa Makao ya Taifa ya watoto tangu mwaka 2001na limewezasha watoto wa kituo hiki kuhakikisha wanapata huduma mbalimbali ikiwemo ustawi wa watoto kiafya na huduma nyinginezo kama vyeti vya kuzaliwa, ujenzi wa mabweni pamoja na huduma za miundombinu ya kituo hicho.
Makao ya Taifa ya watoto wenye shida Kurasini yametembelewa na ujumbe maalum katoka Shirika linalofadhili kituo hiki la Abbot Tanzania ili kujionea Maendeleo ya shughuli za kituo hicho zinazofadhiliwa na shirika hilo.
Akiongea wakati wa kuwakaribisha wageni hao kituoni hapo, Kaimu  Kamishina wa Ustawi wa Jamii Simon Panga amesema Shirika la Abbot Tanzania limekuwa likitoa ifadhili wake kwa kituo hiki tangu mwaka 2001 na kufanikiwa kuleta mageuzi makubwa kwa Maendeleo ya kituo hiki.
Kamishina Panga ameongeza kuwa pamoja na ufadhili was shirika la Abbot Tanzania, serikali imehakikisha huduma muhimu kama vile chakula, malazi, mavazi, matibabu na elimu vinapatikana kwa watoto wote wanaoishi katika Makao ya Watoto Kulasini.
“Watoto huletwa katika kituo hiki kupitia Maofisa wa Ustawi wa Jamii kutoka Hamashauri zote nchini wakiwa na taarifa zilizokamilika kulingana na mazingira waliyotoka na kuanza maisha kituoni hapa kwa ufadhili wa wasamalia na wafadhili kwa kushirikiana na serikali amesema Kamishina Panga.,”
Historia ya kituo inaanza mwaka 1966 pale Wamissionari walipokianzisha kwa lengo la kulea Watoto yatima. Kituo kilianza na  idadi ya Watoto watatu na baadaye kukabidhiwa rasmi kwa serikali ya Tanzania mwaka 1968 na tangu wakati huo serikali ilibadili mfumo wake na kuanza kutoa huduma ya malezi kwa watoto wote wenye shida.

VIGOGO WIZARA MALIASILI, UTALII KORTINI KWA TUHUMA ZA KUSABABISHA HASARA DOLA 32,599

Na Karama Kenyunko, Glogu ya jamii

WAFANYAKAZI watatu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka sita likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya dola 32,599.

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(Takukuru) Leonard Swai, amewataja washtakiwa hao ni, Ofisa Muhifadhi anayehusika na uwindaji wa matumizi endelevu ya wanyamapori Rajabu Hochi, Ofisa wa Muhifadhi mwenye wajibu wa kukusanya wa mapato ya uwindaji , Mohamed Madehele na Isaac Maji.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri imedaiwa kuwa, washtakiwa wakiwa watumishi kitengo cha Wanyamapori, walitenda makosa hayo katika makao makuu ya wizara hiyo.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali Pendo Temu amedai,kati ya Januari 12 na Desemba 31, mwaka 2008, makao makuu ya wizara hiyo, Hochi na Madehele wakiwa watumishi wa wizara hiyo, wakiwa na wajibu wa kukusanya mapato yanayotokana na uwindaji walitumia madaraka yao vibaya kwa kuzidisha wanyama pori kwa Kampuni ya Uwindaji ya Northern Hunting Enterprises (Tanzania) kinyume cha sheria na hivyo kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida ya USD 250 isivyo halali.

Pia Hochi na Madehele, wanadaiwa kati ya Agosti 11 na Desemba 31, mwaka 2011, makao makuu ya wizara hiyo,waliiwezesha kampuni hiyo kujipatia dola za Marekani 250 isivyo halali.Aidha, Hochi na Madehele, wanadaiwa, kati ya Septemba 5 na Desemba 31,mwaka 2010, walishindwa kukusanya faini ya dola za Marekani 15,630 kutoka katika kampuni hiyo.

Pia washtakiwa Hochi na Madehele,wanadaiwa kushindwa kukusanya faini ya dola za Marekani 250 kutoka kampuni ya uwindaji ya Hunting Enterprises (Tanzania), kinyume cha sheria.

Pia kati ya Oktoba 12, 2008 na Desemba 31,mwaka 2011, Hochi na Madehele walishindwa kukusanya mapato yatokanayo na uwindaji dola za Marekani 16,219 kutoka kampuni ya uwindaji ya Hunting Enterprises (Tanzania) na hivyo kuiwezesha kampuni hiyo kupata mapato hayo isivyo halali.

Katika shtaka la sita, washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 12, 2008 na Desemba 31,mwaka 2011, katika makao makuu ya wizara hiyo, wakiwa na wajibu wa kukusanya mapato yatokanayo na uwindaji, waliisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 32,599.

Hata hivyo, washtakiwa wote wamekana mashtaka na wamesomewa masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili watakao saini bondi ya Sh.milioni 50 na mmoja kati ya wadhamini anatakiwa kuweka hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh.milioni 50.


Pia washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na imeahirishwa hadi Januari 31, mwaka huu itakapotajwa tena.

MAAZIMIO YA MKUTANO KATI YA SMZ NA SMT KUSHUGHULIKIA MELI ZINAZOPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KWA TUHUMA ZA KUSAFIRISHA SILAHA NA MADAWA YA KULEVYA, TAREHE 17 JANUARI 2018

Ndugu Waandishi wa Habari, nimewaita hapa kuzungumza nanyi na kupitia kwenu kuzungumza na wananchi wenzangu kuhusu taaarifa ya kukamatwa kwa meli zilizokuwa zimepakia shehena za dawa za kulevya na silaha zikiwa zinapeperusha bendera ya nchi yetu.


Meli hizo ni: 

Kaluba yenye usajili namba IMO 6828753 iliyokamatwa tarehe 27 Desemba 2017 ikiwa na wastani wa kilo 1,600 za dawa za kulevya huko katika maeneo ya Jamhuri ya Dominican Republic; na 

Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa kwa kusafirisha silaha kinyume na Sheria za kimataifa. 

Meli zote mbili zimesajiliwa Tanzania kupitia taasisi yetu ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya kusajili meli za nje.

Hapa kwetu Tanzania tuna aina mbili za kusajili Meli; usajili wa Meli zenye asili ya Tanzania na zile zenye asili ya Nje. kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake mbalimbali, siku zote tumekuwa tunaheshimu na kutekeleza kikamilifu majukumu yetu ya kimataifa yaliyowekwa kupitia mikataba na maazimio mbalimbali ya vyombo hivyo

Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa mkataba wa UNCLOS 1982 kila nchi imepewa haki ya kufanya usajili wa meli kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa na sheria za nchi husika.Kwa upande wa Tanzania, usajili wa meli za kimataifa unasimamiwa na Sheria Na 5 ya mwaka 2006,


(Kwa upande wa SUMATRA ina Merchant Shipping Act ya mwaka 2003. Sheria hi inaruhusu usajili wa meli inayomilikiwa na Mtanzania, au meli inayomilikiwa kwa ubia kati ya Mtanzania na raia wa nchi nyingine. Kwa sheria hii ili meli ipate usajili wa SUMATRA na kuruhusiwa kupeperusha bendera ya Tanzania ni lazima umiliki wa meli uhusishwe na raia wa Tanzania kwa umiliki wote au kwa ubia lakini ni lazima Mtanzania awe na hisa nyingi. Vilevile kampuni hiyo ya umiliki lazima iwe ya Kitanzania kwa maana ya kusajiliwa na kujiendesha kutokea Tanzania hata kama kampuni hiyo inamilikiwa na watu wasio Watanzania. Na kwa upande wa Zanzibar kupitia ZMA wana Maritime Transport Act ya mwaka 2006).

Sheria hii inaruhusu usajili wa meli yoyote hata kama mmiliki wake sio Mtanzania wala kampuni kuwa ya Kitanzania hivyo basi kutoa fursa kwa meli ambayo haina umiliki wa aina yeyote wa Tanzania kwa maana umiliki na ukazi kupewa usajili wa kupeperusha bendera yetu nje ya Tanzania. Aidha, Sheria hizi huendeshwa sambamba pamoja na Sheria na Kanuni za Kimataifa.

Ni vyema tukafahamu kuwa Sheria na Kanuni hizo humlazimu mwenye Meli, kujaza fomu maalumu ya maombi pamoja na Fomu za “DECLARATION OF VESSELS NON INVOLVEMENT WITH CRIMINAL ACTS OR OMISSIONS”; na ndipo hatua nyingine za kufanya uchunguzi wa historia ya meli kupitia International Maritime websites na vyanzo vingine, tangu Meli ilipotengenezwa hadi muda inapoomba usajili.

Uhakiki hufanywa pia kupitia mitandao mingine mikubwa mitatu inayotumika duniani kote kupata historia ya meli, Mitandao hiyo ni:

Fleet Moon; 
Maritime Traffic; na 

iii. Maritime-connector.

Baada ya ZMA ambayo ndio kisheria imeruhusiwa kusajili meli nje ya Tanzania, kujiridhisha na maelezo na taarifa zilizopatikana, maamuzi ya kusajili au kutosajili yanatolewa kupitia Idara ya Usajili.

Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa taratibu za Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya, 1988 na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa 1970 (2011).

nchi zilizosajili Meli zinazokamatwa hutakiwa kutoa kibali kwa Walinzi wa Mwambao wa Bahari wa nchi husika, na kwa Meli hizi, tulitoa kibali kwa Jeshi la Mwambao wa Marekani na Jeshi la Mwambao wa Ugiriki kuzikamata na kuzipekua meli hizo.

Baada ya kupata taarifa za upekuzi hatua za haraka zilizochukuliwa upande wetu ni kufuta Usajili wa Meli hizo.

Ndugu Waandishi wa Habari, Tanzania vilevile ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Vita Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya (United Nations Convention Against Illicit Traffic of Narcotic Drugs and Psychotropic Substance, 1988) na pia ni Mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Vita

Usafirishaji Haramu wa Silaha (United Nations Protocol Against Illicit Manufacturing of and Trafficking in Arms, their Parts and Components and Ammunition, Supplementing the United Nations Convention Against Transnational Organized Crime, 2001).

Kwa mnasaba huu, tunapenda kutoa taarifa kuwa Tanzania imejidhatiti na imedhamiria kutekeleza majukumu yake yaliyoelezwa katika mikataba hiyo ya kimataifa, ikiwemo kushirikiana na mataifa mengine pamoja na mashirika ya kimataifa katika kupiga vita usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha. Nyote ni mashahidi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Tano imetangaza vita dhidi ya watu wote wanaojihusisha na dawa za kulevya na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vinatokomeza kabisa uhalifu huo.

Hivyo basi, taarifa ya kukamatwa kwa meli zenye bendera ya Tanzania zikisafirisha dawa za kulevya na silaha ni kinyume na Sheria za nchi yetu na zile za kimataifa. Taarifa hizi zimeleta mshtuko mkubwa ndani ya nchi yetu. hasa kwa kuwa Tanzania imejipambanua kupambana na maovu hayo kwa kutumia nguvu zote.

Ndugu Waandishi wa Habari, kufuatia taarifa hizo, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliniagiza kuitisha kikao cha dharura baina ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzungumzia kadhia hiyo.
Jana Jumatano, tarehe 17 Januari 2018, Viongozi na Wataalamu wa pande zote mbili wakiongozwa na mimi mwenyewe na Mhe. Balozi Seif Ali Idi, Makamo wa Pili wa Rais, Zanzibar tulifanya kikao kilichojadili masuala haya kwa kina huko Zanzibar.

Ndugu Waandishi wa Habari, baada ya majadiliano ya kina kuhusu masuala haya, kikao kilibaini yafuatayo: 
Suala la Usajili wa Meli za Nje linafanywa na Nchi nyingiduniani; Kwa mfano katika Bara la Afrika 

nchi zinazofanya usajili wa kimataifa ni pamoja na Liberia, Komoro na Sierra Leone. Aidha, kwa Bara la Asia, kuna nchi za China na Singapore na kwa Amerika ya Kusini ni pamoja na Panama.

Ilibainika kwamba Wenye Meli hupendelea kusajili meli zao nje ya nchi zao kwa kukimbia uzito wa kodi na sheria zinazobana shughuli zao. 

Wakala aliyekuwa akifanya kazi hii kwa niaba ya ZMA na ambaye ameshavunjiwa Mkataba bado anaendelea kufanya usajili kwa kuiba Bendera ya Tanzania. 

Kutokana na hayo kikao kiliazimia yafuatayo: 
Kutoa taarifa na ufafanuzi wa kina kuhusu kadhia ya meli hizo kukamatwa na dawa za kulevya na silaha kwa umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla ili kuondoa upotoshaji wa aina yoyote kwa kupitia vyanzo visivyo rasmi. Kwa sasa ndio natekeleza azimio hili; 

Kwa kuwa uendeshaji wa biashara hii unaonekana kuleta utata na kutia dosari kubwa kwa Taifa letu na kuharibu sifa njema za Nchi yetu, imeonekana haja ya kuunda kamati ya pamoja ya wataalam wa SMZ na SMT itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kupitiwa upya usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini mwetu, kuangalia mwenendo mzima wa usajili, na hatimaye kutoa mapendekezo na ushauri kwa Serikali; 

Kuanzisha utaratibu wa kuzifanyia uchunguzi wa kina (due diligence) meli zote mpya zitakazoomba usajili pamoja na wamiliki wake kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vya Serikali vikiwemo vile vya ulinzi na usalama; 

iii. Kufanya mapitio ya sheria zetu, ili kuzipa nguvu zaidi taasisi zinazosimamia usajili wa meli. Wakati wa mapitio ya sheria, timu ya wataalam itaangalia kwa makini kodi zinazotozwa na mchango wake nchini ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili Tanzania;

Kuendelea kushirikiana na nchi nyengine kwa kuzipa ruhusa kukamata na kuzipekua meli zinazopeperusha bendera yetu wakati wote zinapohisiwa kuwa zinafanya uhalifu, au masuala ambayo haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazokubalika kimataifa na wakati wa usajili. 


Asanteni kwa kunisikiliza.